Waziri Mkuu Bwana Mizengo Pinda amesema moja ya majukumu atakayoshughulikia mapema zaidi ni matatizo ya walimu nchini ili kuzuia mgomo mkubwa uliopangwa kufanywa na walimu mwezi Mei mwaka huu.
Akizungumza moja kwa moja na Taasisi ya Utangazaji nchini, TUT, mara baada ya kuapishwa mjini Dodoma katika Ikulu ndogo ya Chamwino juzi, Waziri Mkuu alisema miongoni mwa mambo atakayoshughulika nayo ni pamoja na kuhakikisha ufumbuzi wa matatizo ya madeni sugu ya walimu unapatikana.
Alisema anafahamu kuwa walimu wanaidai Serikali takribani bilioni nane, zikiwa ni fedha za malimbikizo ya mishahara na likizo.
Akaongeza kuwa katika bilioni hizo nane, walimu wa shule za msingi wanadai karibu Sh. bilioni 6.5 huku walimu wa shule za sekondari wakiidai Serikali Sh. bilioni 1.5.
“Kipindi chote Serikali imekuwa ikijitahidi kulipa madeni ya walimu, kitu ambacho itaendelea nacho ili kuhakikisha watumishi wake sekta hiyo wanalipwa madeni yao,“ akasema Waziri Mkuu.
Akaongeza kuwa wakati mwingine wakurugenzi wa Manispaa na Halmashauri wamekuwa chanzo cha madeni hayo, kwani wamekuwa wakitumia fedha za madeni ya walimu katika shughuli zingine.
Alisema kitendo hicho kimefanya walimu kuendelea kuidai Serikali licha ya kujitahidi kutoa fedha kwa ajili ya deni hilo.
Hivi karibuni chama cha walimu nchini (CWT) kilitangaza kuanza mgomo rasmi wa walimu nchi nzima kuanzia Mei mwaka huu kama madai yao hayajatimizwa.
- SOURCE: Alasiri
Filed under: Bongo Habarii!!!











